Wakati mwingine tumekuwa tukiomba sana kwa Mungu lakini hatupokei majibu. Leo
tutajifunza mambo 10 yanayosababisha maombi yetu kutojibiwa.
1)
DHAMBI.
Baada ya mwanadamu kuasi pale Eden dhambi iliingia ulimwenguni na kila
aliyezaliwa alikua na dhambi. Lakini hii haikumaanisha kwamba tukiomba Mungu
hatusikii, bali ilimaanisha ili Mungu atusikie,tulipaswa kwanza kutubia makosa na dhambi zetu ndipo tumueleze Mungu
matatizo yetu.
Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha
Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo.
Yohana 9:31 lakini maovu yenu
yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake
msiuone, hata hataki kusikia.
Hivyo basi kabla hujampelekea Mungu matatizo/shida yako hakikisha
mahusiano yenu yako vizuri.
2) KUKOSA IMANI.
Nadhani hii ni miongoni mwa sababu kubwa inayofanya
watu wasipokee majibu ya maombi yao.
Waebrania 11:6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.
’Hapa ni mchezo wa akili yako na nafsi yako juu ya Mungu unayemuomba na kile unachomuomba. Wakati Yesu alipokuwa anaponya watu, mara nyingi sana aliwaambia ‘Imani yako imekuponya
’(Luka 17:19) kwahiyo
imani ndio msingi wa majibu ya maombi yako kwa Mungu.
Kiwango cha imani yako ndio kitaamua kiasi cha majibu yako kwa Mungu.
3)
KUKATA TAMAA/KUKOSA UVUMILIVU.
Kuna wakati unaweza kusikia mtu akisema, nimeomba vya kutosha Mungu hanisikii,
labda Mungu hanioni. Kauli zote hizi za kukata tamaa hufanya tushindwe kupokea
majibu ya maombi yetu. Habakuki aliambiwa ‘njozi ni kwa wakati ulioamriwa,
na ijapokawia aingojee.
Habakuki 2:2-3
Na muda mwingine majibu yetu yanakuwa yamebeba vitu vikubwa hivyo hukumbana na upinzani mkali, bila kukazana kuomba basi hushindwa kutufikia. Maombi ya Daniel yalizuiliwa kwa siku 21 na mkuu wa anga wa uajemi, kama angekata tamaa basi asingepata majibu ya maombi yake. Daniel 10:12-13.
4)
KUJIKWEZA/KUJIHESABIA HAKI.
Kuna baadhi ya watu hujiona kama vile wao
ni zaidi ya watoto wa Mungu na wana haki zote na hawana dhambi na ni lazima
wapewe kila wanachokiomba. Kama una tabia hiyo, my friend Mungu hatojibu maombi
yako, maana Biblia inasema ajikwezaye atashushwa. Luka
14:11
Yesu aliwahi kutoa mfano wa mfarisayo na mtoza ushuru,
mfarisayo alikihesabia haki alafu mtoza ushuru akajishusha na kujiona mdhambi.
Yesu anasema mtoza ushuru alihesabiwa haki kuliko mfarisayo...
5) KUOMBA BILA KUFANYA KAZI.
Unakuta mtu anaomba Mungu ampe kazi alafu anashinda nyumbani tu bila kutafuta
kazi. My friend, Biblia inasema asiyefanya kazi na asile, kwaiyo kama hufanyi
kazi hata kama unamuomba Mungu hawezi kukubariki/kukujibu maana Mungu anabariki kazi za mikono yetu. Sasa
atabariki nini kama hufanyi kazi? Zaburi 128:2, na 2Thesalonike
3:10
Kuna wakati siyo kuomba tu, lazima kuambatane na kutafuta na kubisha, ili
uweze kuona na kufunguliwa. Luka 11:9
6)
KUTOSAMEHE.
Ndiyo! Kutosamehe waliokukosea ni sababu
mojawapo ya kuzuia majibu ya maombi yako. Maana ili Mungu aweze kukusamehe na
kukusikiliza inapaswa kwanza uwasamehe wengine kama Yeye anavyokusamehe. Efeso
4:32, Mathayo 6:12-15
7) KUOMBA NJE YA MAPENZI YA MUNGU.
Kuomba nje ya mapenzi ya Mungu ni kuomba nje ya utaratibu wa Mungu au kuomba nje ya mipango ya Mungu aliyokuwekea juu ya maisha yako. Utajuaje kama unaomba nje ya mapenzi ya Mungu? ( Tuombe uzima Mungu akinipa kibali nitaandika)1Yohana 5:14
8) KUTOAMBATANISHA NA SADAKA.
Siku hizi ukigusa
ishu ya sadaka tu, watu wanakuwa wakali kama pilipili. Lakini hiyo
haiondoi ukweli wa kuwa sadaka ni muhimu sana katika maombi
yako. Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni.
‘Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako.’ Akujalie kwa
kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote .Zaburi
20:2-4
Na
ukisoma kwenye Biblia sadaka ni kitu cha lazima, ili kuonyesha utii wako mbele
ya Mungu. Lakini hamaanishi basi ukiambatanisha na sadaka unajibiwa, kumbuka
sadaka ya mtu mwovu ni chukizo mbele za Mungu.
Mithali 15:8 Japokuwa sadaka ya kwanza ni moyo wako, na ya
pili ni Damu ya Yesu. Hivyo kama huna sadaka unaweza tumia hizo mbili na Mungu
akajibu maombi yako kwa wakati na bila shida.
9)
KUTAKA KUTUMIA KWA TAMAA.
Wakati mwingine hatupokei majibu ya maombi yetu kwa kuwa lengo letu tukipata ni ili kumtambia fulani,
kumuumiza fulani, kufanyia anasa za dunia nk. Sasa ukiwa na nia hiyo moyoni
mwako Mungu hakujibu. Yakobo 4:3
10)
KUTOMKUMBUSHA MUNGU.
Kumkumbusha Mungu haimaanishi kwamba Mungu anasahau, bali kuna wakati anapenda
Uungu wake uheshimiwe kwa sisi
kumkumbusha ahadi yake kwetu na siyo kukaa tu na kusubiri majibu.
Isaya 43:26 Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate
kupewa haki yako.
Huenda
maombi yako yako mlangoni pako, ni kiasi tu cha kwenda mbele za Mungu
kumkumbusha na kumshukuru nawe
utapokea.
Kama umependa mafundisho haya na unataka kujifunza mengi zaidi bonyeza link hapa chini ujiunge na group la whatsapp - https://chat.whatsapp.com/D3QWYtaZ0864OxdUYSOCUXAsante na Ubarikiwe sana.
IMETOLEWA NA PASTOR ALFA & DANIEL –
CHURCH OF CHRIST - MAJOHE

Comments
Post a Comment